Hali ya afya uliyonayo sasa, yaani, nzuri au mbaya, inatokana na kutoshambuliwa/ kushambuliwa na magonjwa au kuwa na ulemavu wa aina fulani. Na vifo vya mapema, ni matokeo ya mojawapo au zaidi ya mambo yafuatayo:
• Iwapo mmojawapo wa wazazi wako au wote wawili walikuwa “mbegu” nzuri au mbaya ambayo wewe umerithi.
• Umakini au makosa katika kuchagua umri wa mama (mwanamke) kutunga mimba.
• Utunzaji mzuri au mbaya wa kichanga kilicho tumboni (ujauzito au mimba) ikiwa ni pamoja na mjamzito kuwa na tabia na kufanya vitendo hatarishi kwa afya ya kiumbe kilicho tumboni mwake, kwa uzembe, kwa kukosa nidhamu ya maisha, kwa kutojali au kwa kukosa maarifa.
• Umakini au makosa wakati wa mtoto kuzaliwa.
• Utunzaji mzuri au makosa katika utunzaji na malezi ya mtoto aliyezaliwa na katika vipindi vinavyofuata vya siku 1,000 za kwanza, miaka 5 ya kwanza na hadi miaka 14.
• Umakini au makosa ya wazazi na walezi katika kumlisha mtoto aliyezaliwa na kumpatia huduma zote za matibabu, ikiwa ni pamoja na kinga kwa njia ya chanjo za lazima na kupata matibabu yanayotakiwa kwa usahihi na kwa wakati mwafaka.
• Umakini wa wazazi, walezi na, hususan, mayaya, kuzuia watoto wasipate ajali ya kuangukia kichwa (na sehemu nyingine ya mwili), ili wasije wakapata hitilafu katika ubongo na kuwa walemavu au kuwa na matatizo ya afya ya akili.
• Tabia, vitendo na kutojali kwa kijana na mtu mzima katika kujua na kutozingatia kanuni za afya nzuri ambazo ni pamoja na lishe bora, kutojijali na makosa ya kibinadamu au ya kiuzembe ya binadamu wenzake. Mfano mzuri ni vifo vya mapema na watu wengi kuwa walemavu kutokana na makosa ya waendesha vyombo vya usafiri.
• Kutokuwa mcha Mungu.
• Kutojipenda, kutokupenda na kutowajali wanafamilia yako (watoto wa kuzaa na wa kulea na mwanandoa wako), kutokupenda majirani zako na kutompenda Mungu.
Kuna msemo kuwa, “jinsi ulivyo kiafya sasa ni matokeo ya aina ya lishe na ulaji wako, unywaji wako na kujijali au kutojijali.”
Kwa hiyo, uamuzi wa wazazi wako na uamuzi wako mwenyewe, ni msingi mkubwa kwa aina gani ya afya utakayokuwanayo maishani na idadi ya miaka utakayoweza kuishi.
Lakini, suala muhimu hapa si idadi tu ya miaka utakayoishi duniani, lazima, pia, iwe miaka yenye furaha na faida kwa jamii . Unaweza kuishi miaka 90, lakini, kati yake nusu ikawa ya shida na mateso makubwa. Kwanini, basi, uishi miaka 45 ya mwisho?
Kitabu hiki kinalenga kumwelewesha binadamu namna ya kuishi miaka mingi, yenye furaha na faida kwa jamii . Kisome vizuri na fuata kikamilifu uliyojifunza.Uamuzi ni wako peke yako na maisha ni yako, ingawa yanawagusa watu wengi.
Kwa upande mwigine, Mwenyezi Mungu alituumbia mwili tulionao. Mwili huu ni hekalu la Roho yake. Alipotuumba, alitunga kanuni za kuuhifadhi ili usiharibike. Tuliumbwa tuishi miaka mingi duniani. Mwenyezi Mungu hakuumba watoto wafe katika umri mdogo. Alikusudia watu wote wafikie uzee na akawaagiza watoto wawatunze wazazi wao ambao wamezeeka.
Kati ya ‘kanuni’ alizoziweka kulinda mwili ni Amri 10 za Mungu na makatazo mengine yaliyo katika vitabu vitakatifu vya dini, na mafundisho ya viongozi wa dini mbalimbali, wataalamu mbalimbali kama vile, madaktari na ameweka serikali za binadamu ambazo hutunga sheria mbalimbali za kudhibiti tabia na mienendo mibaya ya binadamu.
Mwenyezi Mungu hakuumba magonjwa wala ajali. Vitu hivyo vimeletwa na binadamu mwenyewe kwa:
• Kukaidi Amri zake, makatazo yake na mafundisho yaliyomo katika vitabu vyake vitakatifu.
• Kiburi chake
• Kutozingatia fadhila ya kiasi
• Kutojali kwake
• Kukaidi kutekeleza sheria za nchi ikiwa ni pamoja na za usalama barabarani.
• Kuzembea kuheshimu elimu inayotolewa na wataalam wa afya, madaktari, wataalam wa lishe n.k.
• Kukataa kujielimisha juu ya namna ya kuzuia magonjwa kwa kusoma vitabu, magazeti, majarida, kuhudhuria semina, warsha, mikutano n.k.
• Kukosa kuwa na nidhamu ya maisha.
Mfano mzuri ni, kwa kula vizuri, kunywa kistaarabu, na kudhibiti uzito wa mwili, mtu anakuwa amejikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni ya hatari sana ya shinikizo la damu, moyo, kisukari, ini, figo na saratani za aina nyingi n.k. Maana yake ni kuwa, Mungu hakuumba magonjwa hayo, bali yameletwa na binadamu mwenyewe kwa kushindwa kula kistaarabu (lishe nzuri) na kunywa kilevi kistaarabu kama inavyoshauriwa na wataalam. Hata watoto wanaozaliwa na hitilafu ya mioyo yao, si mapenzi ya Mungu bali ni matokeo ya makosa ya wazazi wao. Waulize madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo. Watasema hivyo.
Si Mungu anayesababisha ajali za magari, gari moshi, pikipiki au ndege bali hitilafu ya vyombo hivyo, hitilafu za njia za usafiri na uzembe na kutojali kwa baadhi ya abiria na waendesha vyombo hivyo. Ajali hizo huangamiza maelfu ya watoto, vijana, watu wazima na wazee. Mungu tunayemwabudu si mkatili, ni mpenda watu wake. Hafurahi anapoona watu wake wanaangamia kwa sababu hizo.
Lengo la kitabu hiki ni kuwarudi binadamu wajipime walipokosea na waone kama wanaweza kujirekebisha ili mii li yao iweze kuishi miaka mingi.
Nguzo 72 Zinazoshikilia Uhai Wako ambazo zinaunda Siri ya Binadamu Kuishi Miaka Mingi, zinalenga kumsaidia binadamu kuishi miaka mingi. Huenda wasomaji watagundua nguzo nyingine. Hakuna lililoharibika. Zote hizo zii shi. Lengo ni lilelile la kuwawezesha binadamu kuishi miaka mingi.
Katika kitabu hiki, wasomaji watajifunza kuwa, wakati umefika wa kuacha kumsingizia Mungu kuwa kila kifo ni “mapenzi ya Mungu,” n.k.
Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, hasa, katika Sayansi ya Matibabu, kuongezeka kwa madaktari bingwa, kuongezeka na kupatikana kwa vifaatiba vya hali ya juu, kama vile, CT scanner, MRI n.k. na kupatikana na kuongezeka kwa aina mbalimbali za dawa katika vituo vya kutolea matibabu, kuongezeka na kusambazwa kwa vituo vya matibabu, kuwapo kwa elimu mpya ya lishe bora, unywaji mzuri, n.k. zote hizi ni fursa mpya za kumwezesha binadamu kuishi miaka mingi. Baadhi ya watoto hawapashwi kuzaliwa na hitilafu za kiafya, watoto na vijana hawapashwi kufa.
Hatuna budi kuachana na ukaidi wa Amri na Makatazo ya Mungu, kutojali, uzembe na tabia ya kutotaka kusoma ii kujiendeleza kwa lengo la kupata maarifa na elimu mpya ya kuishi miaka mingi.
Wakati wote tukumbuke kuwa, Mungu humsaidia mtu anayejisaidia. Usipojihangaikia, Mungu anakuacha ufe kwa ujinga wako.
Nawaalika watu wengi wakisome kitabu hiki ili waweze kuishi miaka mingi. Kufariki uzeeni ni haki ya wahusika. Si kufariki utotoni, ujanani na utu-uzimani kabla ya kusherehekea kumbukizi ya miaka 80 ya kuzaliwa.